CHANGAMOTO ZA VIJANA

Zipo changamoto nyingi wanazozipita vijana katika maisha yao ya kila siku.  Tutaanza kuzichambua moja baada ya nyingine:

Changamoto ya kwanza:

KUJITAMBUA - Mimi ni nani?

Vijana wengi hawajitambui wao ni akina nani na kwanini wanaishi.  Wengi wao wanaishi kwa sababu tu wana uwezo wa kupumua bado.  Matokeo yake vijana wengi hawajui majukumu yako katika maisha yao binafsi hata katika jamii inayowazunguka kiasi kwamba wanajikuta kwamba hawana mchango wowote katika jamii wanazoishi.  Hii inawafanya kujisikia ya kwamba hawana thamani.

KILA MTU NA RIZIKI YAKE

Maisha ya mwanadamu yameshikiliwa na sehemu moja kama ilivyo ndizi katika mkungu. Katika mkungu kuna ndizi nyingi lakini kila ndizi ina nafasi yake ya kukuwa na kunawiri. Hata kama zimebanana vipi hakuna ndizi itakayomnyima mwenzie kukua. Hivyo hivyo na maisha ya mwanadamu, yameshikiliwa na Mwenyezi Mungu, kila mtu ana riziki yake haijalishi unafanya nini. Kikubwa ni kugundua fungu lako ni lipi na kusimama kwenye mstari sahihi ili kufanya mambo sahihi kuweza kupata fungu lako.

JICHO LAKO LA NDANI

.Jicho lako la ndani linaona nini?  Jicho lako la ndani linatakiwa lizione fursa zote zinazokuzunguka.  Ukiruhusu kuona hivyo, hutakosa mbinu za kuzifikia hizo fursa haijalishi unaanguka mara ngapi.

MILIKI NDOTO YAKO

Ndoto hii siyo ile ndoto unayoota ukiwa umelala bali ni ile ndoto inayokunyima usingizi.  Yadhibiti mawazo yako, zidhibiti fikra zako ziswaze au zisione kitu kingine bali ndani yako uwe unaoona hiyo ndoto yako tu.  Kwa kufanya hivi utaakisi vitu vingi vinavyoendana na ndoto yako ambavyo vitakusaidia kufikia ndoto yako.  Hakuna ndoto kubwa, ilimradi unaiona ndani ya fikra zako, basi unaweza kuitimiza